KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesifu juhudi zilizooneshwa na wachezaji wake katika mchezo dhidi ya Coastal Union uliochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam juzi.
Ushindi wa goli 1-0 mbele ya Wagosi wa Kaya uliiwezesha Yanga kufikisha pointi 62 na kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Bara, ikishuka uwanjani mara 24.
Baada ya matokeo hayo, Gamondi, aliwamwagia sifa wachezaji kutokana na kujituma na kuonyesha nini walikuwa wakikihitaji kwenye pambano hilo lililokuwa gumu.
“Kila mchezaji ametimiza wajibu wake ipasavyo, hii ilionesha namna tunavyotaka matokeo kwa kila mchezo”, alisema, Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina, alisema, pia amefurahi kuona washambuliaji wake wakiendelea kuimarika kwa kupunguza papara na anaamini hilo litaongezeka zaidi katika mechi zijazo.
Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umebainisha kwamba umejifunza jambo la muhimu kwenye mchezo huo.
Meneja wa Idara ya Habari Yanga, Ali Kamwe, aliweka wazi kuwa wachezaji walifanya kazi kubwa kusaka ushindi jambo ambalo limewezekana.
“Ilikuwa kazi kubwa dhidi ya Coastal na mwisho tumepata pointi tatu muhimu, tunazidi kufanyia kazi makosa na wametupa somo kuhusu mechi za mwisho ambazo zina ushindani mkubwa.
“Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwa ajili ya mechi ambazo zimebakia, malengo yetu ni kuona kwamba tunafanikiwa kutwaa taji la ligi”.