TEHRAN, IRAN
RAIS wa Iran, Ebrahim Raisi, ni miongoni mwa watu mashuhuri na wa muda mrefu anayeonekana kuwa mrithi wa Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, amefariki kwa ajali ya helikopta katika eneo la milima karibu na mpaka wa Azerbaijan, maafisa na vyombo vya habari vya serikali vilisema jana.
Katika habari za karibuni kabisa viongozi wa ulimwengu wameanza kutuma salamu za rambirambi ambapo Emir Tamim bin Hamad Al Thani wa Qatar ametoa salamu za rambirambi kwa serikali ya Iran na watu wake kwa kifo cha Rais Ebrahim Raisi katika taarifa fupi kwenye mtandao wa X, uliojulikana kama Twitter.
“Rambirambi zangu za dhati kwa serikali na watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kifo cha Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir Abdullahian, na maafisa waliofuatana nao katika ajali mbaya ya helikopta,” Amir alisema kwenye X.
Nae Waziri Mkuu wa India Narendra Modi Jumatatu pia alisema “amehuzunishwa sana na kushtushwa na kifo cha kutisha” cha Raisi baada ya vyombo vya habari vya Irani kuripoti kuwa alikufa katika ajali ya helikopta.
“Rambirambi zangu za dhati kwa familia yake na watu wa Iran,” Modi alichapisha kwenye X, zamani Twitter. “India inasimama na Iran katika wakati huu wa huzuni.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohamed Shia al-Sudani alisema nchi yake inaunga mkono watu na viongozi wa Iran kufuatia tukio hilo la kusikitisha, kwa mujibu wa taarifa rasmi.
“Kwa masikitiko makubwa, tumepokea taarifa za kusikitisha za kuaga dunia Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ibrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje, Hossein Amir Abdollahian, na maafisa wao wakuu, kutokana na ajali mbaya ya ndege huko kaskazini mwa Iran,” waziri mkuu wa Iraq alisema.
“Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu, Ali Khamenei, na kwa taifa la Iran, serikali yake na watu wake. Tunaelezea mshikamano wetu na watu ndugu wa Irani na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu wakati wa msiba huu mkubwa,” iliongeza taarifa hiyo.