NA SAIDA ISSA, DODOMA
SERIKALI imesema kuwa katika mwaka 2024/25, wizara ya Habari, Mawasilino na Teknolojia ya Habari, imepanga kutekeleza maeneo mbalimbali katika usalama wa mtandao ikiwemo kutengeneza mkakati wa ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wanaofanyiwa mitandaoni.
Waziri wa wizra hiyo, Nape Nnauye alieleza hayo alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25, ambapo aliomba na kuidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 180.9.
Waziri Nape aliendelea kutaja maeneo watakayo yafuatilia mitandaoni kuwa ni pamoja na Kusimamia usajili na usimamizi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA nchini, kuanzisha Kituo kimoja cha usalama wa mawasiliano cha Taifa,
“Kuhuisha mfumo wa takwimu za makosa na matukio ya mtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na Mahakama, kuongeza uwezo wa Kitengo cha Uchunguzi wa kidijitali kwa Jeshi la Polisi katika ofisi ya makao makuu ya Dar es Salaam na kanda ya Zanzibar”, alisema.
Kadhalika waziri huyo alisema kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ina wajibu wa kusimamia mapinduzi ya kidijitali nchini, Mapinduzi ya Kidijitali yanaweka msingi wa kulipeleka Taifa kwenye Uchumi wa Kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA.
Ili kuharakisha Tanzania kuelekea katika uchumi wa kidijitali, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanza kutumika kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Kanuni zake pamoja na uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi,”alisema.
Alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa mapinduzi ya kidijitali yanachochewa na matumizi ya taarifa (Data) ambayo imekua ni bidhaa adimu.
Pia alisema kuwa Serikali imepitisha Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali 2024-2034 utakaosaidia kuongeza matumizi ya kidijitali kwa huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na sekta binafsi.
“Mkakati huo una nguzo muhimu sita zikiwemo uwezeshaji wa miundombinu ya kidijitali, utawala wa kidijitali na uwepo wa mazingira wezeshi, kujenga uelewa na ukuzaji wa ujuzi wa kidijitali, uwepo wa utamaduni wa ubunifu wa kidijitali na teknolojia wezeshi”, alisema.