Watall waliokwama katika hifadhi ya Masai mara kutokana na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa wameokolewa.
Hoteli, nyumba za wageni na kambi zimejaa maji kutokana na mafuriko, ambapo mamlaka nchini humo zililazimika kutumia helkopta kuwaokoa watalii hao waliokwama kwa siku kadhaa.
Nyumba wanazokaa watalii zimejaa maji baada ya mto ulio ndani ya mbuga ya Maasai mara kuvunjika kingo na hivyo maji kusambaa katika hoteli na nyumba za wageni katika mbuga hiyo.
Hifadhi hiyo ilipo kusini magharibi mwa Kenya, ni kituo maarufu sana kwa watalii kwa sababu ya mandhari yake na kuwa na idadi kubwa ya nyumbu ambao wanaotokea Serengeti nchini Tanzania.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema limewaokoa watu 36 kwa njia ya usafiri wa anga na wengine 25 kwa njia ya barabara.
Serikalli ya kaunti ya Narok imesema imepeleka helikopta mbili kuwabeba watu wanaoondolewa katika eneo hilo la hifadhi.
Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko nchini Kenya imefikia 181.
Kulingana na shirika la kutoa msaada la msabala mwekundu, maelfu ya watu wamekoseshwa makaazi nchini humo kutokana na mafuriko.
Watu 48 walifariki Mai Mahiu, katikati mwa Kenya na shughuli za uokoaji na kutafuta miili inaendelea kwa kutumia mbwa wa kunusa.
Maofisa wa shirika la msalaba mwekundu wanaendelea kuwasaidia wakaazi wa Kitengela, kilomita 33 kutoka Nairobi ambao nyumba zao zimejaa maji, pamoja na kuwaokoa watalii katika mji wa Narok, kilomita 215 kutoka Nairobi.