Skip to content

Wanakijiji zaidi 20,000 Ileje waja juu waichongea RUWASA

SONGWE

BAADHI ya wananchi wa vitongoji vya kijiji cha Itumba kata ya Isongole wilayani Ileje mkoani Songwe. wamewalalamikia watendaji wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira (RUWASA) kukwamisha mradi wa maji uliotolewa fedha Bil,4.9.

Wilaya ya Ileje inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa maji safi kwa baadhi ya maeneo ambapo siku za hivi karibuni bilioni 4.9 zilitolewa lakini mradi wa maji umekwama hadi sasa.

Wakizungumza kwenye mkutano wa Mkuu wa Mkoa huo, Daniel Chongolo, katika uwanja wa Itumba walisema wanashangazwa kuona mradi huo mkubwa kukwama na wameomba kupatiwa majibu kujua hatma ya mradi huo.

Edwain Hakim mkazi wa Itumba alisema  anaomba timu ya uchunguzi  kutoka nje ya Wilaya iundwa kuuchunguza mradi huo na kama kuna ubadhirifu hatua za kisheria zichukuliwe, kwani Bilioni 4.9 ni fedha nyingi hawaoni sababu ya mradi kukwama alafu serikali ikawa kimya.

Baada ya malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alimuinua Meneja wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), Mhandisi Andrew Tesha, Wilayani Ileje, kujibu malalamiko hayo, ambapo alikiri mbele ya mkutano mradi huo kuwa na shida.

Alisema mradi huo wa Itumba Isongole una  thamani ya Bilioni 4.9 ambao ukikamilika watu 20,888 watanufaika na tenki la lita milioni 3 linajengwa mradi upo asilimia 85 utakuwa na ziada ya maji.

Mkuu wa mkoa Chongolo, baada ya majibu hayo ya Injinia ,alisema anajibebesha suala hilo ili kujua tatizo ni nini na kwamba Rais Dk, Samia Suluhu katoa Bilioni 4.9 ili wananchi wake waondokane na kero ya maji, leo mradi unakwama akiahidi kupata majibu sahihi.