WATOTO wengi kwenye malezi hujikuta wakikabiliwa na unyanyasaji kutoka kwa walezi wao kwenye familia.
Katika familia nyingi hapa nchini watoto wengi wamepitia mambo magumu ya ukatili wanaofanyiwa na wazee wao wa kambo.
Hapa napenda ifahamike kuwa sina maana kwamba wazee wote wa kambo ni wakatili dhidi ya watoto wanaoishi nao, lakini kwa asilimia kubwa watoto hao hupitia kwenye malezi magumu yanayoambatana na ukatili.
Mara nyingi watoto wanaolelewa na wazazi wa kambo hupitia unyanyasaji ambao humfanya mtoto kuvunjiwa sheria kuhusu haki za mtoto.
Watoto wa namna hiyo, hupata athari za kimwili, kimaadili na kihisia ikiwemo vipigo, kutukanwa matusi, kubaguliwa, kutojaliwa unyanyasaji wa kingono na utumikishwaji.
Bila shaka wazazi wawe wa kambo ama wengine na hata walezi wa watoto wanapaswa kutambua kuwa malezi wanayowapati watoto ndiyo yanayowajenga fikra za maisha yalivyo.
Acheni ukatili katika maonyo yenu kwa watoto. Kumbuka mtoto anajifunza kwa vitu anavyofanyiwa.
Mtoto anaanza kujua matukio tangu akiwa tumboni mwa mama yake, hivyo wazee nawasihi jifunzeni kutia elimu kwa mtoto kabla hajazaliwa, kama msingi bora wa upeo wa mtoto.
Adhabu kwa mtoto hazikatazwi ila ni lazima ziwei na viwango. Mtoto wa miaka miwili hawezi jengwa kwa adhabu sawa na ile itolewayo kwa mtoto wa zaidi ya miaka sita.
Nashauri wazazi kupitia hatua zifuatazo pindi wanapoona kosa kwa watoto wao, kwanza wamfundishe mtoto jinsi gani ya kufanya mambo mazuri.
Kama kafanya jambo ambalo ni kinyume mkanye asirudie tena, jaribu kuwa naye karibu na upime mwenendo wa vitendo vyake.
Jaribu kumuhoji utapata kujua hisia zake, lakini pia mambo ambayo yapo kwenye moyo wake.
Unapaswa kumuadhibu mtoto, lakini uwe umeshapitia hatua kadhaa za kumfundisha kumkanya, hata hivyo unapaswa kumpa adhabu inayolingana na hali yake.
Baada ya kumwadhibi, mkumbushe tena, kisha umsisitizie athari za kulirudia kosa. Kuna makosa ambayo mzazi lazima aelekee kwenye adhabu moja kwa moja.
Mzazi unapaswa kuzingatia kuwa kabla ya kuadhibu watoto ni vizuri ukahakikisha unaifahamu vyema afya yake. Hii itakusaidia kuchagua na aina ya adhabu itakayomfaa mtoto.
Wapo walezi wengine wanaokurupuka kutoa adhabu kwa watoto bila hata kuuliza hali ya kiafya ya mtoto.
Kumbuka watoto katika zama za sasa sio mali ya familia pekee, bali ni wa jamii husika. Kila mtu anahusika kwenye malezi ya mtoto katika jamii bila kuzingatia uhalali wake na inafaa zaidi kuwasiliana na mzazi husika au kutoa taarifa za kosa husika kwa wazazi.
Wazazi wawe na tabia ya kuweka kumbukumbu ya makosa wanayofanya watoto wao ili kufahamu hatma na mienendo ya watoto.
Wazazi msikimbie wajibu wa kulea watoto kwa kusingizia majukumu. Kumbuka mtoto umleavyo ndivyo akuavyo na jukumu la kulea si la mama pekee, bali la wazazi wote.
Tutumie lugha ya upole wakati wa kuzungumza na watoto, ukali uliopitiliza huweka hofu kubwa kwa mtoto na kumfanya akose kujiamini.