NA SAIDA ISSA, DODOMA
SELIKARI pamoja na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini wameafikiana kusimamia maazimio 15 ambayo ndani yake serikali imetoa maagizo kwa taasisi husika.
Akizungumza na waandishi Dodoma, Thobias Makoba Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, alisema maazimio hayo ni pamoja na Maamlaka ya Mapato Tanzania TRA kusitisha zoezi la ya kamata kamata.
Alisema TRA inaagizwa kuweka mfumo mzuri utakaowezesha utoaji wa nyaraka muhimu za manunuzi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini kuanzia Julai, 2024. Aidha, utekelezaji wake utawekewa utaratibu mzuri kwa kushirikisha wadau wote muhimu.
Ameeleza kuwa Serikali inaiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania kuongeza haraka Bandari Kavu (ICD) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo kupitia utaratibu wa de-consolidation.
Aidha TRA imeelekezwa kuongeza nguvu kwenye kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi na maboresho ya kodi yanayofanyika ili kuwezesha kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi nchini huku Taasisi husika za Serikali pamoja na mabaraza ya biashara yashirikishwe kikamilifu katika ngazi zote.
TRA pia inaelekezwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika. Bidhaa hizo ni vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti.
Serikali kwa ujumla itaendelea na zoezi la kuwapanga na kuwawekea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo ambao hawako kwenye maeneo rasmi ili kurahisha usimamizi, ufuatiliaji na urasimishaji wao wa biashara.
Aidha, katika kipindi cha muda wa kati, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya viwango vya kodi tulivyo navyo kwa sasa ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa amani na haki kulingana na thamani ya biashara zao.
Vilevile, katika kipindi cha muda mfupi na wa kati, Serikali itashughulikia changamoto zote za wafanyabaishara zilizowasilishwa Serikalini hususan zile ambazo hazihitaji mabadiliko ya sera au sheria;
Wataalam wa TBS na TRA kwa pamoja wameelekezwa kukamilisha marekebisho ya mfumo wa TEHAMA ili mizigo inayoingia nchini kwa njia ya uchangiaji makasha iweze kugombolewa kwa namba ya usajili wa mlipakodi (TIN) ya mwenye mzigo badala ya TIN ya wakala bila ya kuwa na gharama za ziada kwa mlipakodi ambapo zoezi hili linatarajiwa kukamilika Julai, 2024,” alisema.
Alibainisha, Serikali imeelekeza Wizara ya Fedha kuratibu zoezi la kufanya uchambuzi, tathmin na mapitio ya mfumo mzima wa utozaji na ukusanyaji pamoja na viwango vya Ushuru wa Huduma (Service Levy) pamoja na kushauri njia mbadala ya utozaji itakayo kuwa rafiki zaidi kwa wafanyabiashara ili kulinda mitaji na ukuaji wa biashara nchini.
Kuhusu wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na mamlaka zingine husika itaendelea kuimarisha ukaguzi wa vibali vya kazi kwa wageni ili kuhakikisha kuwa wamiliki wa vibali hivyo wanafuata masharti ya vibali hivyo kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Alisema Mawaziri wanaohusika na sekta ya biashara watakutana na wafanyabiashara wote nchini kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wafanyabiashara pamoja na kupokea maoni yatakayolenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini wakati wote.
Alieleza Wataalamu wa Forodha wakutane na Jumuiya ya Wafanyabishara nchini mara moja ili kujadiliana kuhusu taratibu za kiforodha hususani uthaminishaji na ugomboaji wa mizigo. Suala hili likamilike ifikapo tarehe 10 Julai, 2024.
Pia alisema Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) itaendelea kuratibu suala la kutoa mrejesho kwa wafanyabiashara kila robo mwaka kuhusu utekelezaji wa mazimio baina ya wafanyabiashara na Serikali.
Kutokana na maazimio hayo na maagizo ya Serikali, pande zote mbili zimekubakiana hali ya biashara kote nchini kuendelea kama kawaida ili kuwapa watanzania huduma wanazostahili.