Skip to content

Wadau wapongeza ongezeko bajeti ya kilimo

  • Bara

WABUNGE na viongozi mbalimbali wametembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa na wizara ya Kilimo yaliyopo katika viwanja vya bunge jijini Dodoma na kutoa maoni yao kuhusu sekta ya kilimo katika kuelekea kuhitimishwa kwa bajeti ya wizara hiyo.

Akizungumza katika viwanja hivyo, mbunge wa viti maalum Sophia Mwakagenda alimpongeza Dk. Samia kwa kuongeza bajeti ya kilimo kwani zaidi ya asilimia 60 ya wananchi ni wakulima.

Alisema bajeti hiyo ikitekelezeka na fedha zikatumiwa na kukubalika kwenda katika maeneo husika maendeleo makubwa yatapatikana katika sekta ya kilimo. 

“Kupitia bajeti hii fedha hizi zikielekezwa katika maeneo makubwa nina uhakika sekta ya kilimo itakuwa na maendeleo makubwa sana, bajeti hii pia imezungumza utafutaji wa masoko nchi za nje kwa ajili ya wakulima wetu”, alisema.

Alisema pamoja na hayo waziri husika amejitoa sana katika kilimo hali inayosababisha sekta hiyo kupiga hatua na kwamba tija kwenye kilimo imeanza kuonekana.

“Tunachomuomba waziri asimamie uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama vile chai, kahawa na mazao mingine, lakini pamoja na bajeti kuongezwa ni lazima ashuke chini”, alisema.

Naye Elizabeth Bolle,  meneja ununuzi wa mbolea kutoka mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania alimpongeza Dk. Samia kwa kuleta Mapinduzi ya kilimo nchini kwani dhamira hiyo imedhihirika kutokana na uwekezaji mkubwa wa rasilimali fedha katika sekta ya kilimo. 

Alisema kuwa kwa mwaka 2022/23, serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia gharama za kununua mbolea na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao kwa lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.

Kwa upande wake Justa Katunzi afisa kilimo mkuu wa wizara ya Kilimo, alisema kuwa huduma za ugani kwa sensa ya mwaka 2019/20 zinaonesha kuwa wastani wa asilimia 6.9 ya wakulima wanapata huduma za ugani.

Alisema kuwa juhudi za serikali za kuongeza uwekezaji katika kuimarisha huduma za jamii ikiwemo kilimo ambapo kumeongezwa upatikanaji wa vitendea kazi kwa maofisa ugani ikiwemo pikipiki.

“Tumenunua vifaa vya kupimia udongo ili wakulima waweze kutumia mbolea kulingana na mahitaji yaliyopo katika udongo wao, tunanunua vishikwambi ili kusudi maofisa ugani waweze kuwasiliana na wakulima kupitia simu zao za mkononi”, alisema ofisa huyo.