RAIS wa Kenya, William Ruto amewataka madaktari kusitisha mgomo huku serikali ikijitahidi kutimiza matakwa yao kwadiri ya hali ya kifedha itakavyoruhusu.
Katika hotuba yake ya siku ya wafanyakazi kwenye bustani ya Uhuru Gardens jijini Nairobi, Ruto aliwaambia madaktari kuwa serikali haiwezi kutimiza matakwa yao yote kikamilifu kutokana na matatizo ya kifedha.
“Tumewasilisha kile ambacho serikali iko tayari kufanya; 17 kati ya madai 19, mengine hayawezekani kwa sasa kwa sababu ya matatizo ya kifedha”, alisema.
“Nawaomba madaktari warudi kazini, tutasuluhisha, turekebishe uchumi na kila mtu atapata haki yake siku za usoni. Lazima tuwe waaminifu kwa kila mmoja hata kama inauma, hakuna haja ya kusema uongo”, alisema Ruto.
Tangu Machi 14, madaktari wamekuwa kwenye mgomo na kupinga hatua ya serikali kushindwa kuwapa madaktari mkataba wa majadiliano ya Pamoja (CBA) wa 2017 kuhusu masharti ya kazi ya madaktari.