NA MWANDISHI WETU
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Eliakimu Mnzava amewashukuru na kuwapongeza viongozi na wananchi wa mkoa wa Mjini Magharibi kwa kutekeleza kwa vitendo shughuli za serikali zikiwemo za mbio za mwenge.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mwenge katika ya uongozi wa mkoa huo na mkoa wa Kaskazini Unguja, Mnzava alieleza kuwa wameridhika na ushirikiano uliooneshwa na viongozi wa ngazi mbali mbali na wananchi katika utekelezaji na usimamizi wa miradidi na programu zote zilizofikiwa na mwenge.
Alisema kutokana na hamasa iliyooneshwa na wananchi wa mkoa huo kuna uwezekano wa kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa na kuamini kuwa uwepo wa mwenge katika mkoa huo utaongeza ari ya utendaji kazi wa kila mmoja katika nafasi yake.
“Kama walivyotangulia kueleza wenzangu, nikiri kuwa tumeridhika na jinsi mlivyojipanga kukimbiza mwenge hasa katika usimamizi wa miradi inayotekelezwa na serikali nahata ile ya sekta binafsi”, alieleza Mnzava.
Awali akiasilisha taarifa ya mkoa huo kabla ya kuukabidhi mwenge na wakimbiza mwenge kwa mkuu wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Hadid Rashid Hadid, Mkuu wa mkoa wa mjini magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, alieleza kuwa kupitia mikesha ya Mwenge wwananchi wamehamasishwa kufanya vipimo mbali mbali ili kujua afya zao.
Alieleza kuwa jumla ya wananchi 1,381 (Magharibi ‘B’’ 579, Mjini 534 na Magharibi ‘A’ 268) walifanyiwa uchunguzi wa VVU na ugonjwa wa Malaria ambapo watu 838 walifanyiwa uchunguzi wa VVU na wananchi 543 wamechunguzwa Malaria.
“Kati ya waliochunguzwa VVU, watu watatu waliogundulika na watu wa watatu waligundulika na malaria vile vile jumla ya chupa za damu 109 zimepatikana kutoka kwa wananchi waliojitokeza kuchangia”, alieleza Kitwana.
Aidha Kitwana aliwashukuru wakimbiza Mwenge Uhuru na Mkufunzi wao kwa ushirikiano na kazi kubwa waliyoifanya walipokuwa mkoani humo ambapo walipitia kwa kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 140.7.
Akipokea mwenge huo, hadid alieleza kuwa utakapokua mkoani kwake, mwenge utakimbizwa kwa wastani wa kilomita 89 kwa kukagua, kuweka mawe ya msingi kwenye miradi na programu mbali mbali zinazoendana na ujumbe wa mwenge mwaka huu.
Aidha aliahidi kuukimbiza na kufikisha ujumbe wa mwenge katika maeneo mbali mbali ya wilaya za mkoa huo kwa kuanzia wilaya ya Kaskazini ‘A’ ambapo mkesha wa mwenge utakuwa Pwani Mchangani.
Mbio za mwenge kitaifa 2024 zilianza mnamo mwezi Aprili mwaka huu mkoani kilimanjaro ambapo ulianza kukimbizwa katika mkoa wa Mjini Magharibi Mei 17, mwaka huu ukitokea mkoa wa Kaskazini Pemba na kuanzia wilaya ya Magharibi ‘B’, Mjini na kumalizia Magharibi ‘A’ jana.