KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na matamshi juu ya baadhi ya mataifa kuhusu uwezekano wa kutumia silaha za nyuklia katika migogoro ya kijeshi, vitisho ambavyo havipaswi kuchukuliwa kama mzaha.
Rais Vladimir Putin wa Urusi, mnamo mwezi Machi mwaka huu, hakuacha kuelezea kwamba nchi yake ipo tayari kutumia silaha za nyuklia ikiwa kutakuwepo tishio kwa serikali na uhuru wake.
Kauli ya Vladimir Putin ni kama onyo la wazi kwa nchi za magharibi ambazo kwa kiasi kikubwa zimejitolea kuisaidia Ukraine kwenye mapambano ya kivita yanayoendele.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha serikali ya Urusi, Putin alimuelezea Joe Biden wa Marekani kama hatari zinazoweza kutokea ikiwa mzozo utatanuka, lakini akasema kuwa hafikirii kuwa ulimwengu unaelekea kwenye vita vya nyuklia.
Hata hivyo, Putin alisisitiza kuwa vikosi vyenye dhamana ya silaha za nyuklia vya Urusi vimejitayarisha kikamilifu huku akisema kuwa mifumo ya silaha za nyuklia ya Urusi iwe ya angani, majini na ardhini ni bora zaidi.
“Kwa mtazamo wa kijeshi na kiufundi, bila shaka, tuko tayari kwa vita vya nyuklia. Wanajeshi wa Urusi daima wako katika hali ya utayari wa kupambana, hili ndilo jambo la kwanza. Pili, kwa ujumla, mifumo yetu ya nyuklia ni ya kisasa zaidi kuliko mingine yoyote. Ni sisi tu na Marekani ambao tuna mifumo kama hii. Lakini mifumo yetu ni ya kisasa zaidi”, alisema Putin.
Kiongozi huyo wa Urusi mara kwa mara amekuwa akielezea juu ya utayari wa nchi yake kutumia silaha za nyuklia tangu alipoivamia Ukraine mwezi Februari mwaka 2022.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa haamini kwamba dunia inaelekea kwenye vita vya nyuklia. Kulingana na Umoja wa Mataifa, Nyuklia ndio “silaha hatari zaidi duniani,” kwa wakati huu.
Urusi ilirudia tena uwezekano wa kutumia silaha za nyuklia hasa baada ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kuelezea utayari wake wa kupeleka wanajeshi nchini Ukraine kusaidia kwenye vita dhidi ya Urusi.
Urusi pia imefikiria tena matumizi ya silaha za nyuklia hasa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, David Cameron kuiambia Ukraine kwamba makombora iliyopewa na taifa hilo yanaidhini ya kutumika kusambulia ndani ya ardhi ya Urusi.
Msemaji wa serikali ya Urusi, Dmitry Peskov alisema kauli za hivi majuzi za rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron ni duru mpya kabisa ya kuongezeka kwa mvutano.
Silaha za nyuklia zipo je? Silaha hizi zipo katika mfumo wa mabomu na makombora na kwamba zinatumia nishati ya nyuklia ili kusababisha ili mlipuko.
Ukubwa wa mlipuko unaosababishwa na bomu la nyuklia unaweza kuathiri mfumo wa mwadamu wa kusikia, kuharibu ngozi au hata kupofusha macho kutokana na mionzi mikali inayotoka baada ya mripuko.
Athari za muda mrefu ya milipuko ya bomu la nyuklia hushuhudiwa pia husababisha kuchafuka kwa tabaka la ozoni na hivyo kuwaweka binadamu kwenye hatari zaidi.
Mlipuko mmoja wa nyuklia una uwezo wa kuteketeza mji mzima ndani ya muda mfupi tu. Mara ya mwisho kutumika kwa silaha hizi ilikuwa ni wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia, ambapo Marekani ilishambulia miji miwili ya Hiroshima na Nagasaki iliyopo nchini Japan.
Katika mashambulizi hayo, zaidi ya watu 140,000 walipoteza maisha huku asilimia zaidi ya 90 ya makaazi yaliharibiwa katika mashambulizi hayo.
Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa unakadiria uwepo wa silaha za nyuklia zipatazo 13,400 na majaribio 2,000 ya silaha za aina hiyo.
Kutokana na hatari ya silaha za nyuklia, mwaka 1946 Umoja wa Mataifa uliunda tume ya kudhibiti matumizi ya silaha hizo wakati wa migogoro ya kijeshi.
Mikataba mitano ya kimataifa dhidi ya matumizi ya silaha za nyuklia imeanzishwa tangu wakati huo, ikiwemo mkataba wa kuzuia silaha za nyuklia.
Kwa nini silaha za nyuklia ni hatari sana? Pindi zinapolipuka, silaha za nyuklia hubadilisha mfumo wa kawaida wa hewa na kusababisha joto kali la kufikia nyuzi joto milioni 15.
Joto hilo lina uwezo wa kusababisha majeraha vidonga vikubwa kwenye mwili wa binadamu, hata kwa umbali wa kilomita 30 lilipododoshwa bomu hilo.
Wimbi la mlipuko wa nyuklia huwa na uwezo wa kusafiri maelfu ya kilomita kwa saa, jambo ambalo husababisha madhara kwa sehemu kubwa ya watu, viumbe hai vyengine na kuharibu mazingira.
Mwanga wa mlipuko wa nyuklia ni zaidi ya mara sita ya ule unaotoka kwenye jua na kuongeza uwezekano wa kupofusha mtu aliye umbali wa hata kilomita 80.
Athari za muda mrefu ya milipuko ya nyuklia pia husababisha kuchafuka kwa tabaka la ozoni na hivyo kuwaweka binadamu kwenye hatari zaidi.