Skip to content

Fainali CRDB Federation Cup ni Yanga Vs Azam

NA MWANDISHI WETU 

YANGA imetinga fainali ya CRDB Federation Cup baada ya kuilaza Ihefu goli 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili, uliochezwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. 

Goli pekee la Yanga lililofungwa na Stephane Aziz Ki kunako dakika ya 101, akiunganisha krosi safi ya kiungo, Pacome Zouzoua, na kuamsha shangwe la mashabiki uwanjani hapo. 

Pambano hilo lililazimika kuchezwa kwa dakika 120 baada ya miamba hiyo kuzimaliza dakika 90 za kawaida wakiwa hawajafungana. 

Yanga ambayo ndiyo watetezi wa michuano hiyo, walianza mchezo kwa kasi huku ikiongozwa na Khalid Aucho, Maxi Mpia Nzengeli na Pacome Zouzoua kwenye kiungo na kuiweka Ihefu katika majaribio mengi. 

Lakini, Ihefu ilitulia na kuidhibiti Yanga huku ikifanya mashambulizi ya hatari kwenye lango la wapinzani wao na kupoteza nafasi kadhaa. 

Yanga sasa itakutana na Azam FC kwenye fainali itakayopigwa Juni 2 mwaka huu katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati, Mkoa wa Manyara. 

Matajiri wa Dar, Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo, walifanikisha lengo la kutinga hatua ya fainali kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union. 

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Azam FC walikuwa wababe ndani ya dakika 90 pekee. 

Magoli mawili yalifungwa na Abdul Sopu kunako dakika ya 42 kwa mkwaju wa penalti na la pili ilikuwa dakika ya 79. 

Kiungo, Feisal Salum alipachika bao moja kwenye dakika ya 68 kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa. 

Kocha, Miguel Gamondi, alisema, wapo tayari kwa mchezo wa fainali na kuhakikisha wanatwaa tena ubingwa huo.

Aidha, aliwapongeza wachezaji wake kutokana na kupambana kwa dakika zote 120 za pambano hilo. 

“Tunatambua utakuwa mchezo mgumu, lakini, tupo tayari kwa kuwa wachezaji wanapenda kushinda na wamekuwa wakipambana juu ya hilo”.