DAR ES SALAAM,
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema sekta ya viwanda ni muhimu katika ukuaji wa uchumi jumuishi kwa kuongeza uzalishaji, kutoa ajira kwa wananchi na kusadia kuondosha umasikini.
Kauli hiyo alitoa jana, wakati akizindua kiwanda cha kuzalisha gari cha ‘Saturn Corporation Limited’ katika eneo la viwanda, liliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji ndiyo maana imeimarisha mazingira ya uwekezaji na kuwa rafiki zaidi, hivyo kampuni kutoka sehemu mbalimbali duniani zinakaribishwa kutumia fursa ya uwekezaji.
Dk. Samia alieleza kuwa uzinduzi wa kiwanda hicho ni utekelezaji wa mpango wa tatu wa miaka mitano wa maendeleo ambao umejielekeza katika uchumi wa viwanda.
Alifahamisha msingi wa mpango huo ni ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, ambayo imetoa maelekezo ya kujenga uchumi wa kisasa fungamamishi, jumuishi na shindani kupitia viwanda, pia uchumi huo uendane na huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.
Alisisitiza kuwa serikali inazingatia ahadi ya ilani hiyo kwa namna mbali mbali ikiwemo kujenga na kuimarisha miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege na ujenzi wa meli ili kurahisisha usafiri na usafishaji.
Akijibu ombi la bomba la gesi kwa kampuni hiyo, Dk. Samia alisema shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), linatekeleza mpango wa kufikisha gesi asilia kwa kutumia gari hadi watakapojenga kituo kidogo Kigamboni ili viwanda viweze kupunguza gharama za matumizi ya nishati ya umeme.
Dk. Samia alisema tayari wazo hilo wanalo TPDC, la kujenga kituo kidogo kitachokuwa Kigamboni, ambapo mpango huo utakapokamilika mwezi Februari mwakani ambapo kutakuwa na mageuzi makubwa kwenye sekta ya nishati.
Katika hatua nyengine, Dk. Samia alimtaka waziri wa Viwanda na Biashara kuhakikisha mnyororo wa uwekezaji wa viwanda haukatiki na wawe na kubadilishana kutoka mzalishaji mmoja kwenda kwengine.
Sambamba na kuwasisitiza waziri wa Viwanda pamoja na Waziri wa Uwekezaji waregeze masharti na wapunguze urasimu wawekezaji ili viwanda vijengwe kwa wingi na vijana wapate ajira.
Alisema vipuri vinavyotumika kuunganisha gari katika kiwanda hicho ni takribani 2400, kwa sasa vingi vinatoka nje ya nchi, hivyo wanaweza kunufaika zaidi kupitia uzalishaji wa viwanda vyengine vya vipuri vya magari, mitambo na mambo mengine hapa nchini.
Pia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutafuta hekta 50 ili waweze kuwasiliana na waziri wa Ardhi ili wajuwe wanachoweza kufanya, ambapo alisisitiza kukabidhiwa kwa hekta hizo utaendana na kupata mpango kazi kutoka katika kampuni hiyo kwa ajili ya kukabidhiwa ardhi na kuweza kufuatiliwa.
Alisema ili kuchochea uwekezaji wa viwanda, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inabidi wawezesha viwanda vinavyozalisha na vyengine kama inavyoelekeza mifumo ya serikali kusomana katika kutekeleza sera ya viwanda ipo haja kwa waziri huyo kuhakikisha viwanda wenyewe vinasomana ili kujua nani anazalisha nani.
Kwa upande wake, waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alisema sekta ya viwanda na biashara ndio msingi wa uchumi wa taifa, na kumpongeza Dk. Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya kipindi cha miaka mitatu katika kuhakikisha wawekezaji wa viwanda wanaingia nchini.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema takribani kwa miongo mitatu uchumi wa Tanzania umekuwa ukikuwa vizuri na ukichangiwa sana na kilimo, huduma pamoja na uwekezaji wa miundombinu, ambao serikali umefanya.
Alieleza kwa takwimu za mwaka jana, katika miradi 526 ambayo iliyosajiliwa na TIC kati ya hyo miradi 237 ilikuwa katika sekta ya viwanda ambayo hiyo imetokana na maono ya Dk. Samia ya kujenga sekta hiyo.
Mapema Mkurugenzi wa Saturn Corporation Limited, Rehmatullah Habib Mouna alisema kampuni hiyo inaunganisha magari makubwa kama Tipa, Treta, ambacho kimeanza kazi mwezi Machi mwaka huu na mpaka sasa wameshazalisha gari karibu 150, ambazo zipo kiwandani hapo na baada ya uzinduzi huo watayauza.