Skip to content

Dk. Mwinyi: Tutaendeleza ujenzi skuli za kisasa

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema nia ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuendeleza ujenzi wa miundombinu itakayosaidia kuharakisha maendeleo.

Dk. Mwinyi alieleza hayo katika uwanja wa Jamuhuri uliopo katika skuli ya sekondari Utaani Wete, wakati alipofungua skuli ya sekondari ya wanawake yenye ghorofa tatu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mwinyi alisema ujenzi wa miundombinu ya kisasa ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu ndiyo utakaoharakisha maendeleo.

Alifahamisha kuwa ujenzi wa skuli hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya serikali iliyoitoa baada ya tukio la moto lililoteketeza skuli ya awali iliyokuwa na madarasa 11 na kuahidi kujenga skuli bora zaidi ambayo  ina madarasa 41.

Aidha, Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuahidi ujenzi wa dahalia kubwa ya kisasa itakayoendana na hadhi ya skuli hiyo mpya.

Dk. Mwinyi aliiagiza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kusimamia ujenzi uliobakia wa ukumbi wa mikutano na uwanja wa michezo utakaoendana na hadhi ya muonekano mzuri wa skuli hiyo.

Aliridhia ombi la wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba la kuimarishiwa skuli ya Jadida kueleza kwamba serikali itajenga skuli mpya ya msingi ya ghorofa pamoja.

Alisema katika hatua ya kuimarisha hadhi ya kisiwa cha Pemba, serikali kupitia Shirika la Nyumba (ZHC), itafanya ukarabati wa nyumba za maendeleo za kisiwa hicho au kujenga nyumba mpya 4,000.

Akizungumzia bandari ya Wete, aliwaeleza wananchi wa kisiwa Pemba kwamba serikali pia imedhamiria kujenga bandari ya kisasa ya Wete ambapo hatua za awali za ujenzi wa bandari hiyo zimekamilika.

Kwa upande wake, waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhammed Mussa, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya elimu.

Naye mwakilishi wa jimbo la Wete, ambae pia ni waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Harusi Said Suleiman, alisema ujenzi wa skuli hiyo ni fursa ya kukuza elimu katika jimbo hilo.

Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa skuli hiyo ya sekondari Utaani, katibu mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said alisema ujenzi wa skuli hiyo ulianza mwezi Mei mwaka jana na hadi kukamilika umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.2.

Alisema skuli hiyo ya kisasa ina jumla ya madarasa ya kusomea 41, ofisi nne za walimu, ofisi ya mwalimu mkuu, vyoo 32, maktaba, maabara, chumba cha kompyuta na stoo.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatibu alisema, wananchi wa mkoa huo sasa wanajali zaidi maendeleo na wameachana na siasa za zamani za chuki.

Serikali imelazimika kuijenga upya skuli ya sekondari Utaani kufuatia kupata ajali ya kuunga moto ulioteketeza kila kitu mnamo mwezi Machi mwaka 2022.