Skip to content

Hamas kusitisha mazungumzo iwapo Rafah itashambuliwa

GAZA, PALESTINA

KUNDI la Hamas la Palestina limesema mazungumzo ya kusimamisha mapigano na Israel yatasitishwa iwapo Israel itaushambulia mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Ofisa mwandamizi wa kundi la Hamas, Osama Hamdan ameishutumu Israel kwa kutaka kuzitisha pande zote kwa madai ya kushambulia Rafah na kusisitiza kwamba, kundi lake bado lina nguvu za kivita la kutetea watu wake.

Habari zinasema, waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema Israel itaingia Rafah na kuwaondoa wapiganaji wa kundi la Hamas walioko huko bila kujali kama itafikia makubaliano na Hamas ama la.

Kutokana na kauli hiyo ya Netanyahu, Hamas imesema kuwa endapo Rafah itashambuliwa hakutakuwa na mazungumzo ya kutafuta amani.

Huku hayo yakiendelea Marekani imesema kuwa imedhamiria kutaka kumalizwa vita baina ya Israel na Hamas na kwamba kuna haja ya kuwepo makubaliano.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, alisema “hata katika nyakati hizi ngumu, tumedhamiria kupata usitishaji wa mapigano kuwarudisha mateka nyumbani”.