Skip to content

Wataalam vipimo zingatieni uadilifu – Mazrui

WAZIRI wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, amewataka wataalamu wanaohusika na vipimo vya DNA kuwa waadilifu na waaminifu wakati wanapofanya majukumu yao.

Mazrui alisema hayo ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-Wakili Kikwajuni wakati akizungumza na wataalamu, wafanyakazi wa afya na wanafunzi kwenye siku ya mkemia Mkuu wa Serikali.

Alisema wagonjwa wanaokwenda kutafuta majibu ya vipimo hivyo imani yao kupata majibu sahihi yatokanayo na vipimo, hivyo uaminifu kwa wataalamu wanaotekeleza jukumu hilo kuwa waadilifu ili kuongeza imani kwa wagonjwa.

“Maabara za vinasaba zipo duniani kote lazima muwe waaminifu na waadilifu kuepusha udanganyifu na teknolojia hii inatoa majibu sahihi ambayo huongeza imani kwa wananchi pale wanapopatiwa majibu ya vipimo vyao”, alisema.

Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa vinasaba sio kujua matatizo ya binaadamu pekee, bali kuongeza uzalishaji kwenye mazao ya matunda na viungo pamoja na uzalishaji wa wanyama.

Sambamba na hayo alisema vinasaba husaidia kujua watu sahihi waliopata ajali kwenye sekta ya anga na baharini kila yanapotokea majanga, hivyo aliwanasihi wataalamu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kufanya uchunguzi kupitia maabara hizo za DNA.

Mazrui aliwasisitiza wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kuongeza wataalamu watakaofanya kazi kwenye maabara kuongeza wataalamu kwenye eneo hilo.

Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya nane inaendelea kujenga hospitali na maabara kubwa zitakazofanya vipimo vya aina tofauti na kueleza kwamba majengo hayo yanahitaji wataalamu watakaofanya uchunguzi kupitia maabara hizo.

“Hatuwezi kuagiza watu kutoka nje kuja kufanya utafiti katika Nchi yetu wakati vijana wanaoweza kufanya kazi hiyo tunao”, alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wizara ya Afya, Dk. Habiba Omar Hassan, alisema vinasaba husaidia kujifunza utaalamu wa kilimo kurahisisha uzalishaji.

Alisema teknolojia hiyo inatumika kuhusisha uhusiano wa kifamilia na kujua vinasaba kujua mtoto halali alizaliwa na familia gani.

Nae Mkurugenzi Kinga kutoka wizara ya Afya, Dk. Msafiri Marijani alisema kipimo cha DNA humjua muhalifu atakaebakisha chembechembe za jasho kwa mtu aliyefanya uhalifu na kujua mtu sahili aliyefanya uhalifu.

Alisema katika kuona umuhimu wa kipimo hicho hapa Zanzibar, wizara itaendelea kutoa elimu kwa jamii kuendelea kutumia vipimo vya vinasaba kupata uhalisia wa vizazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano kutoka wizara ya Afya, Khamis Rashid Kheri alisema DNA imekuwa na umuhimu mkubwa katika kupata utaalamu wa viwango vya dawa za asili ambazo hutumiwa na jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *