MAOFISA nchini Israel wanazidi kuwa na wasiwasi juu ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC), kupanga kutao hati ya kukamatwa kwa viongozi wa kijeshi na kisiasa nchini humo kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.
Ripoti kutoka nchini humo zinabainisha kwamba waziri mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu anaweza kuwa miongoni mwa watu wanaotolewa hati ya kukamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama hiyo kwa kuhusika na tuhuma za uhalifu dhidi ya bidaadam.
Mahakama ya ICC, yenye makao yake makuu mjini The Hague nchini Uholanzi, kwa muda sasa inachunguza hatua za Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu miaka mitatu iliyopita.
Mahakama hiyo pia inachunguza tuhuma za vitendo vya uhalifu dhidi ya binaadam katika vita inavyoviendesha Israel huko Gaza dhidi ya Wapalestina.
Kwa mamlaka iliyonayo mahakama hiyo ya kimataifa inao uwezo wa kuwashtaki na kuwahukumu watu binafsi kwa makosa makubwa zaidi chini ya sheria za kimataifa.
Itakumbukwa kuwa mahakama hiyo iliwahi kutoa hati za kukamatwa kwa viongozi kadhaa akiwemo Vladimir Putin wa Urusi, Muammar Gaddafi wa Libya na mbabe wa kivita nchini Uganda Joseph Kony.
Kutokana na hali ya wasiwasi kuzidi kwa viongozi wa Israel, waziri mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu kama kawaida yake ameishutumu mahakama ya ICC kwa kujaribu kulemaza uwezo wa Israel wa kujilinda.
Hatu ya Netanyahu kutoa kauli hiyo inaonesha wazi kwamba nyuma ya pazia kuna jambo linajadiliwa dhidi ya Israel ambayo imekuwa na mienendo ukiukwaji wa haki za binadaam na uhalifu katika maeneo ya Wapalestina huku ikisaidia na Marekani na mataifa ya magharibi.
Ingawa ICC haijathibitisha madai ya Israel, Mwendesha Mashtaka mkuu wa mahakama hiyo, Karim Khan alipotembelea Israel na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu mwezi Disemba mwaka jana ujumbe wake ulikuwa wazi kwa kile alichokishuhudia.
Khan ambaye ni wakili kutoka nchini Uingereza alizuru maeneo ya mashambulizi ya Hamas katika vijiji vya Israel karibu na uzio wa Gaza, ambapo wapiganaji wanaoongozwa na Hamas walivamia Oktoba 7 mwaka jana.
Aidha mwanasheria huyo alikutana na viongozi wa kisiasa na alisafiri hadi Ramallah kuzungumza na familia za waathirika wa Palestina kuhusu waliyoyapitia huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.
“Wahusika wote lazima wafuate sheria za kimataifa za kibinadamu”, alifafanua katika taarifa yake wakati huo. “Ikiwa hutafanya hivyo, usilalamike wakati ofisi yangu inapohitajika kufanya kazi.”
Khan alisema mashambulizi ya Oktoba 7, ambapo watu wenye silaha wakiongozwa na Hamas waliwaua takribani watu 1,200, wengi wao wakiwa raia na kuwakamata mateka 253, waliwakilisha uhalifu mkubwa wa kimataifa.
Katika kisa cha Israel, mahangaiko yake yalikuwa mawili. Alisisitiza wajibu wa kuendesha operesheni yake ya kijeshi huko Gaza kulingana na vigezo vya wazi vya kisheria vinavyosimamia migogoro ya silaha.
Israel imeshutumiwa kwa kushindwa kuwalinda raia vya kutosha wakati wa mashambulizi yake ya miezi kadhaa ya mabomu, ingawa inasisitiza kuwa inachukua hatua zote zinazohitajika kuepusha majeruhi.
Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas katika eneo hilo inasema zaidi ya watu 34,500 wameuawa huko tangu vita kuanza na kwamba wengi wa idadi hiyo ni wanawake na watoto.
Khan pia alisisitiza haja ya msaada wa kibinadamu kuingia Gaza na upatikanaji wa chakula, maji na vifaa vya matibabu ni haki ya msingi kwa raia bila kuchelewa.
Pia aliwataka Hamas kutogeuza au kutumia vibaya vifaa hivyo pindi wanapofika, baada ya shutuma za Israel kwamba wanachama wake walikuwa wakipora malori na kuiba misaada, hivyo basi kuizuia kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Israel si mwanachama wa ICC na inasema mahakama hiyo haina mamlaka nayo, lakini mahakama imeamua kwamba tangu 2015 ina mamlaka juu ya Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki na Gaza baada ya Wapalestina kuridhia mkataba wake wa kuanzisha, mkataba wa Roma, kama mamlaka ya Palestina.
Hakuna demokrasia ya mtindo wa kimagharibi ambayo imepewa waranti ya kukamatwa kwa kiongozi wake hapo awali, ikitokea kwa Netanyahu, atakuwa wa kwanza.
Michael Oren alikuwa balozi wa Israel nchini Marekani kati ya 2009 hadi mwaka 2013, aliashiria kuwa kesi ya hivi karibuni iliyoletwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo iliishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki dhidi ya wakazi wa Palestina huko Gaza, shutuma kali dhidi ya Israel.
Mnamo Januari mwaka huu mahakama ilitoa uamuzi wa muda ambao uliiamuru Israel kuchukua hatua za kuzuia mauaji ya halaiki huko Gaza, lakini ikaacha kuwaambia ikomeshe mashambulizi yake ya kijeshi.
Michael Oren alisema viongozi wa Israel hawapaswi kushikiliwa na kwa hakika ni pigo kwa hadhi ya nchi hiyo kimataifa na usalama wa nchi hiyo. Kwa sababu nchi ambayo viongozi wake wanaotuhumiwa kuongoza uhalifu wa kivita, nchi hiyo iko hatarini zaidi.
Sir Geoffrey Nice, wakili mwingine wa Uingereza, aliongoza mashtaka ya rais wa zamani wa Serbia Slobodan Milosevic kwa uhalifu wa kivita katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Yugoslavia ya zamani (ICTY).
Anadokeza kuwa hatua za pande zote mbili katika mzozo huu zimo ndani ya muelekeo wa ICC. “Uchunguzi wowote hautakuwa tu kuhusu jeshi la Israel na uongozi wa kisiasa na kijeshi, lakini pia Hamas.
Pia alizungumzia mapendekezo kwamba ICC inaweza kuwa chini ya shinikizo la kisiasa kufikiria upya maamuzi yake. “Serikali kote ulimwenguni, hasa serikali kubwa na zenye nguvu, ziko kulinda masilahi ya nchi yao.
“Kwa hivyo ikiwa wanaona kesi inakuja, au uchunguzi … hiyo itawasababishia kama nchi uharibifu mkubwa wa sifa na ikiwa wanadhani wanaweza kuingilia kati kesi au mchakato wa upelelezi au kesi ili kuwaokoa kutokana na uharibifu huo wa sifa, basi watafanya hivyo, kwa sababu wanatenda kwa maslahi ya nchi yao.”
Muda wa kutoa vibali unaweza kutofautiana, kwa wiki na hata miezi wakati mwingine hupita kati ya hatua ambayo mwendesha mashtaka wa ICC anaomba, na majaji wakubali.
Wakati mwingine maelezo yanaweza kuwekwa siri ikiwa itachukuliwa kuwa kuyaweka hadharani kunaweza kupunguza uwezekano wa kukamatwa.
Hatua kama hiyo dhidi ya Netanyahu na wenzake wa kisiasa au makamanda wa kijeshi wa Israel itakuwa na athari za vitendo pia.
Itaathiri uwezo wao wa kusafiri kote, kwani mataifa ya mkataba wa Roma yanalazimika kuwakabidhi watu wanaowatembelea wakiwa na waranti dhidi yao. Hata hivyo, baadhi ya mataifa hayo yamepuuza waranti za ICC katika miaka ya hivi karibuni.
Balozi wa zamani wa Israel Michael Oren anaamini athari ya baadaye itakuwa pana zaidi, kubadilisha simulizi ya jamii ya Israel.