Skip to content

Buyern Munich yamnyemelea Erik Ten Hag

LONDON, England

ERIK TEN HAG hatofanya mazungumzo na Bayern Munich hadi msimu wa Manchester United utakapomalizika, kwa mujibu wa ripoti.

Bayern wamekabiliwa na vikwazo vingi katika jitihada zao za kuchukua nafasi ya Thomas Tuchel mwishoni mwa msimu huu huku Xabi Alonso, Julian Nagelsmann na Ralf Rangnick wakikataa kujiunga na timu hiyo.

Kwa mujibu wa Sky Sports, Bayern sasa wamewasiliana na wakala wa Ten Hag ili kujadili uwezekano wa kupatikana kwa Mholanzi huyo msimu huu wa joto.

Hata hivyo, ripoti hiyo inadai kuwa Ten Hag ameweka wazi kwa mwakilishi wake kwamba lengo lake pekee ni kwenye msimu uliosalia wa United, ambao unajumuisha mechi nne za ligi kuu ya Uingereza pamoja na fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City mnamo Mei 25.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa Ten Hag ‘anafahamu’ maslahi ya Bayern, ingawa hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika.

Wakati huo huo, Ten Hag amepuuzilia mbali mapendekezo kwamba anahisi hatari katika nafasi yake huko United kufuatia kuondoka kwa mkurugenzi wa soka John Murtough na mtendaji mkuu Richard Arnold.

‘Hapana, sina hisia hizo, nafanya nao kazi vizuri, tumelingana, tunawasiliana kila siku, alisema Ten Hag.

Bayern pia wameweka wazi kuwa wanamtarajia Tuchel kuondoka mwishoni mwa msimu huu, Klabu ilichukua hatua mwishoni mwa Februari na kufikia makubaliano.